Mada: Haki za mtoto katika mazingira ya kidigitali

Kila mwaka Juni 16, ulimwengu huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Afrika. Siku hii ilianzishwa mwaka wa 1991 na Shirika la Umoja wa Afrika (OAU) kuadhimisha uasi wa Soweto wa mwaka 1976, wakati maelfu ya wanafunzi weusi nchini Afrika Kusini walipopinga utawala wa ubaguzi wa rangi na sera zake za elimu. Tangu wakati huo siku hii maalum inakusudia kuongeza ufahamu kuhusu changamoto na fursa ambazo watoto wa Afrika wanakabiliwa nazo, hasa katika maeneo ya afya, elimu, na ulinzi.

Kulingana na ripoti ya UNICEF, zaidi ya nusu ya vifo vya watoto ulimwenguni hutokea barani Afrika, hasa kwa sababu za lishe duni, malaria, nimonia, na magonjwa ya kuhara[1]. Mtandao wa Africa Research, Implementation Science, and Education (ARISE) ulianzishwa mnamo 2014 kwa lengo la kujenga na kudumisha uwezo wa afya ya umma barani Afrika. Mtandao huu huunga mkono utekelezaji wa Lengo la 3 la Maendeleo Endelevu ya dunia(SDG 3), ambalo linatafuta kuhakikisha maisha yenye afya na kukuza ustawi kwa watu wa umri wote[2]. Mtandao huu husaidia kufikia malengo haya kwa kufanya utafiti, kutoa elimu, na kuwezesha ushirikiano kati ya wataalamu wa afya na taasisi za Kiafrika. ARISE inajumuisha taasisi 21 katika nchi tisa za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo zinashirikiana kwenye mifumo ya afya na sayansi ya utekelezaji, na Africa Academy for Public Health (AAPH), taasisi yenye ubora katika eneo hili, ndio mratibu wa Mtandao huu.

Idadi ya watumiaji wa simu za mkononi na mtandao duniani kote ilifikia bilioni 4.95 mwanzoni mwa mwaka 2022, ongezeko la milioni 192 (4%) kutoka mwaka uliopita, na vijana ndio watumiaji wakubwa[3]. ARISE imeanza kufanya ubunifu na majaribio ya teknolojia ya kidigitali kwa ajili ya ufuatiliaji na utekelezaji wa afua mbalimbali kwa vijana. Katika moja ya miradi mkoani Tanga, Tanzania ambapo vijana wapatao 1300 wanaohudhuria na wasiohudhuria shule, teknolojia ya simu za mkononi ilitumika kukusanya taarifa na kutoa elimu ya lishe ili kuongeza ujuzi na ubora wa lishe kwa vijana. Taarifa za uchunguzi wa awali na wa mwisho wa mradi huu zilinyesha matokeo chanya ya afua hii. Matokeo haya yanaonyesha moja ya fursa ambazo teknolojia ya kidigitali inaleta kwa ustawi wa Mtoto wa Kiafrika.

Kwa mujibu wa dhima ya mwaka huu, "Haki za mtoto katika mazingira ya kidigitali", ni muhimu kuelewa kwamba mtandao na teknolojia nyingine za kidigitali huweza kuwa na faida nyingi kwa watoto kama vile kujifunza, burudani na kuongeza ushirika katika jamii. Hata hivyo huweza pia kuleta hatari fulani kama vile uonevu mtandaoni, matapeli wa mtandaoni na habari potofu. Ili kuhakikisha kwamba watoto wanaweza kufurahia faida za ulimwengu wa kidigitali wakiwa wanaepuka hatari. Tukiwa tunasherehekea Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Afrika mwaka huu, ni muhimu kuongeza ufahamu juu ya fursa na changamoto ambazo teknolojia inawezaleta kwenye ustawi, maendeleo na ulinzi wa watoto wetu. For Better Public Health

 


[1] Child and youth mortality data ages 5-24 - UNICEF DATA

[2] THE 17 GOALS | Sustainable Development (un.org)

[3] Digital 2022: Global Overview Report — DataReportal – Global Digital Insights

Source Name: 
Dr. Mariam Ngaula